Wazazi waambiwa wawapeleke wanao shuleni hata kama kuna mgomo wa waalimu


Wazazi wamehimizwa kutofeli kuwapeleka watoto shuleni kutokana na mgomo wa waalimu unaoingia siku ya pili leo na kuhakikishiwa kuwa suluhu ya kudumu itapatikana na wanafunzi kurejelea masomo yao hivi punde.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Nakuru Victoria Mulili, Wizara ya Elimu imeweka mipangilio maalum kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaoenda shuleni wanapokelewa vyema na kuendelea na masomo yao.

Mulili aliendelea kusema kuwa tayari waalimu wakuu katika shule za upili ambapo waalimu wamegoma, wameshapokea ujumbe kushughulikia wanafunzi hadi pale hali hii itakapo rudi shwari.

Aliwahimiza wanafunzi hasa wale ambao wanatarajia kufanya mtihani wa kitaifa mwisho wa muhula huu kujikaza kisabuni na kuendelea na masomo yao kwa sababu wana muda mchache uliosalia kuufanya mtihani huo.

Miungano ya waalimu ya KNUT na KUPPET ilinuia kufanya mgomo wao kwanzia hapo jana lakini KNUT walijiondoa Jumapili jioni wakisema kuwa wameelewana na serikali kupitia kikao cha mazungumzo ya kwamba baadhi ya matakwa y
ao yatashughulikiwa kikamilifu.

Source: Kenya News Agency